Bishop Sylvester Gamanywa |
“Heri ninyi
watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa
ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa
mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”
(MT.5:11-12)
Maneno mazito ni haya ya “watakapowashutumu…….na
kuwaudhi……..na kuwanenea……. Kila NENO BAYA kwa UONGO….” Kuna kushutumiwa
na kulaumiwa na kunenewa vibaya lakini kwa mambo ya kweli, kwa makosa
ya kweli. Hii ni kawaida kila mkosaji kulaumiwa kwa makosa yake.
Lakini si rahisi, na si kawaida, mtu asiye na hatia kabisa,
kushutumiwa, kulaumiwa na kunenwa vibaya kwa tuhuma za kashfa za uongo.
Tena tuhuma ambazo wahusika wanawea mikakati ya makusudi huku wamepania
kwa makusudi kumdhalilisha, kumvunjia heshima yake, huyo asiye na hatia
“maskini wa Mungu” ili tu aabike, aadhirike, aharibikiwe, na ikiwezeka
afilie mbali!!!
Kisa ni nini? Ati kwa kuwa tu yeye ni “mchaji
Mungu”! Ati anawakera mno kwa kuwa ni “mshika maadili ya kibiblia”! Ati
kwa kuwa kajitoa mhanga kutangaza habari za imani yake aliyo nayo kwa
Mungu wake!!!
Tena wengine wamemkasirikia kwa madai ati
“anajifanya mtakatifu sana, hataki kushiriki maovu; hatoi wala kupokea
rushwa; kajitenga na ufisadi kwa sababu ya imani yake kwa Yesu!” Basi,
kwa ajili hiyo tu, zinasukwa njama na kutengenezwa tuhuma za kashfa za
uongo dhidi yake; ili tu kumkomoa na kumkomesha asiendelee na msimamo
wake wa kimaadili. Haya ndiyo Yesu alimaanisha aliposema, “….na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo KWA AJILI YANGU..”
Sasa uzito
wa ujumbe huu sio kusingiziwa na kuzushiwa kwa ajili ya imani. Uzito wa
ujumbe huu ni jinsi “mtendewa, msingiziwa, mzishiwa,” anavyoagizwa jinsi
ya kuchukuliana na hali ya namna hii. Anaagizwa na Yesu kwamba AFURAHI
NA KUSHANGILIA AKITUNGIWA KASHFA ZA UONGO KWA AJILI YA KRISTO!
Hapooooo!!! Kufurahi na kushangilia!!!!
“Ee Bwana Yesu nisaidie
miye mtu dhaifu sanaa naomba unirehemu tu katika hili! Ninatamani kupata
thawabu zako, ila kwa thawabu hii ninahitaji neema yako. Maana udhaifu
wangu huu unaweza kunikosesha hata thawabu nyingine nisipokuwa makini
sana katika eneo hili..AMINA” Duh! Samahani kwa kusali hadharani lakini
najua ujumbe huu una walengwa wake.
Napenda kuhitimisha kwa
kusema ya kwamba, tuache unafiki, ukweli inauma sanaaaa kunenwa vibaya
kwa uongo. Lakini ni kwa sababu ya maumivu ya jinsi hii ndiyo maana Yesu
naye kaweka njia ya kupona maumivu hayo. Anatutaka tuwe na mtazamo
tofauti pale tunapopatwa na majaribu ya jinsi hii.
Kwanza kila
unaposingiziwa kwa uongo, na wewe unajua kuwa huo ni uzushi, kumbuka
shahidi wako wa kwanza ni Mungu. Wakati watu wengine wasiojua ukweli
wanatapokuwa wanakulaumu na kukutukana kwa kashfa ambazo chanzo chake
sio wewe; kumbuka, laani zao zitageuka kuwa baraka kwako mbele za Mungu.
Lakini ili baraka hizo zidumu lazima kwanza uishinde hisia ya
uchungu na maumivu ya nafsi, kwa kuwasamehe bure wale wanaokuudhi.
Unaishinda hisia hiyo hasi ya uchungu? Kwa kuruhusu hisia chanya ya
furaha, na hata kushangilia kwa ajili ya THAWABU KUBWA INAYOKUSUBIRI
MBINGUNI.
Msomaji wangu, usikubali kumaliza mwaka huu ukiwa na
uchungu moyoni kwa sababu ya kashfa za uongo. Sisi sote tutakuna siku
moja mbele za Kiti cha hukumu cha Kristo na ukweli utajulikana wakati
huo. Hivi sasa furahi na kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa hayo
ndiye mapenzi yake pale tunapoteswa isivyo haki….. “Maana huu ndio wema
hasa, mtu akivumilia kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivya haki.”
(1 Pet.2:19)
Nakutakia baraka za Krismasi na mwaka mpya. Kama
ujumbe huu umekugusa nijulishe kwa ku-like na pia warushie marafiki zako
wengine wapate kupona kiroho. Ubarikiwe sana!
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon