Bishop Sylvester Gamanywa |
MAANDIKO YA MJADALA
"Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike
walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa
ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho
yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama;
basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako
duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa
binti za wanadamu, wakazaa nao wana; hao ndio waliokuwa watu hodari
zamani, watu wenye sifa." (MWA.6:1-4)
Katika maandiko haya ziko
kambi mbali mbali za malaika ambazo zinakinzana kuhusu habari za "wana
wa Mungu"; "binti za wanadamu", na "Wanefili"!
Hata hivyo katika
mada hii nitazichambua kambi mbili kubwa na kutoa ufahamu wangu kwa
kadiri ninavyo yafahamu maandiko kuhusu maana sahihi ya mambo yanayoleta
utata kwenye maandiko hayo
NADHARIA WA “WANA WA MUNGU” KUWA NI “MALAIKA WA MUNGU”
Kambi ya kwanza ya nadharia maarufu sana ni hii inayofundisha ya kwamba
"wana wa Mungu" wanaotajwa kwenye MW. 6:1 ni "malaika wa Mungu
walioasi" kwa “kuacha enzi yao” na kuamua kuoana na "binti za wanadamu"
ambapo matokeo yake ni kuzaa "watoto wa kinefili au wanefili". Nukuu za
maandiko yenye kutumiwa na Nadharia hii kutetea madai ya "wana wa Mungu"
kuwa ni "malaika wa Mungu walioasi” ni kama ifuatavyo:
Ayub1:6-7; "Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda
kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. BWANA
akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na
kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku
na huku humo."
Ayub 2:1: "Tena kulikuwa na siku hao wana wa
Mungu walipokwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda
kati yao, ili kujihudhurisha mbele za BWANA."
Yud.1:6 "Na
malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao
yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa
hukumu ya siku ile kuu."
Hayo ndiyo Maandiko maarufu
yanayotumika kutetea nadharia ya "wana wa Mungu" kuwa ni "malaika wa
Mungu walioasi" na kwamba Mungu aliamua kuwafungia kuzimu kwa "kushindwa
kulinda enzi yao"!
NADHARIA YA “WANA WA MUNGU” NI BINADAMU WA “UKOO WA SETHI”
Kambi ya pili ya “nadharia pinzani” na maarufu katika mjadala huu
yenyewe inafundisha ya kwamba, "wana wa Mungu” waliotajwa katika MW.6:1
“sio malaika wa Mungu walioasi” bali ni binadamu wa ukoo wa Sethi ambaye
ndiye chumbuko binadamu walipoanza kuliitia jina la BWANA
Nadharia hii inapinga dhana ya "wana wa Mungu" kuwa si malaika walioasi kwa sababu Yesu alisema "malaika hawaoi"! MT: 22:30-31;
UCHAMBUZI WANGU KUHUSU MW:6:1-4
Kama ilivyo kawaida yangu, kabla ya kuwasilisha uchambuzi wangu, kwenye
mijadala tata kama hii huwa sifuati mkumbo wa kinadharia wa “wengi wako
wapi” bali "kweli ni nini na iko wapi"! Kwa hiyo mimi nami nimefanya
utatifi binafsi wa kimaandiko pamoja na kuchunguza misamiati ya maneno
yaliyotumika katika mukhtadha wa kile mwandishi wa Kitabu cha Mwanzo
alichokuwa anakilenga kuhusu historia ya binadamu.
Baada ya
kujiridhisha ndipo nilifikia kukubali kwamba "wana wa Mungu" waliotajwa
katika Mw. 6:1 sio "malaika wa Mungu walioasi"; na nukuu za "wana wa
Mungu" kuwa ni "malaika wa Mungu" katika Ayub 1:6:2:2 hayana uhusiano na
Mw 6:1 na nukuu za maandiko ya Yuda kuhusu “malaika walioiacha enzi yao
(Yud.1:6) haikulenga kisa cha Mw.6:1
UTETEZI WANGU KUHUSU "WANA WA MUNGU" SI "MALAIKA WA MUNGU WALIOSI"
Nianze kwa kusema ya kwamba Mwandishi wa Mw.6:1 ambaye ni Musa hakutoa
hii tafsiri ya kwamba hao aliowataja kuwa ni "wana wa Mungu" kuwa ni
"malaika wa Mungu"! Kwa hiyo, madai ya wana wa Mungu ni "malaika ni
dhana ya kufikirika"!
Nilipochunguza kwa makini mukhtadha wa
mwandishi wa kitabu cha Mwanzo niligundua kilicholengwa sio "uasi wa
malaika" bali ni "uasi wa binadamu" kwa sababu zifuatazo:
i)
Malaika kwa asili hawana jinsia ya kuoa na kuolewa inayowaruhusu
“kujitwalia wake wo wote waliowachagua..” Maneno haya yanawahusu
binadamu ambao wana maumbile na uhuru wa kuchagua kuoa.
ii)
Ghadhabu ya Mungu haikuwalenga haiwalengi "malaika" bali "binadamu":
"....Roho yangu haitashindana na mwanadamu kwa kuwa naye ni nyama....".
Hakuna mantiki makosa wafanye “malaika wa Mungu” halafu ghadhabu ya
Mungu iwashukie wanadamu ambao kimsingi wao ndio waathirika wa
kuingiliwa kingono na malaika hao.
Ushahidi mwingine mzito wa
kimaaandiko unaonishawishi nikubali kwamba "wana wa Mungu" waliotajwa
katika Mw.6:1 sio "malaika wa Mungu walioasi" ni haya yafuata:
"Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi
leo nimekuzaa? Na tena Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu
mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na
wamsujudu malaika wote wa Mungu. Na kwa habari za malaika asema,
Afanyaye malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto.
Lakini kwa habari za Mwana asema, Kiti chako cha enzi, Mungu, ni cha
milele na milele; Na fimbo ya ufalme wako ni fimbo ya adili." (EBR.
1:5-8)
Kwa maandiko haya tunathibitisha ya kwamba "hakuna mahali
popote" katika maandiko ambapo "Mungu amemtakia na kumteua malaika
yeyote kuwa ni mtoto wake"!
Badala yake tunasoma ya kwamba Mungu
amewaumba malaika katika asili ya kuwa viumbe wa kiroho (si kama
wanadamu wenye miili ya kuoa na kuolewa); na nafasi yao mbele za Mungu
ni "watumishi wake tu"!
Utetezi wangu wa pili ni wa maneno ya
Yesu mwenyewe pale aliposema "...katika kiyama ya wafu watu hawaoi wala
kuolewa bali huwa kama malaika mbinguni.." (MT.22:30-31)
Japokuwa
katika mukhtadha wa maandiko Yesu alikuwa akibanisha ya mbinguni hakuna
kuoa na kuolewa kama duniani; bado mfano kuhusu "malaika wa mbinguni"
kuwa hawaoi ni ushahidi ya kwamba malaika hawakuumbwa na miili yenye
jinsia yoyote ya kike wala kiume!
Utetezi wangu mwingine ni
kukanusha maandiko ya "malaika ambao walishindwa kulinda enzi yao...."
kwenye waraka wa Yuda (Yud.1:6) kuyahusisha maandiko haya na kisa cha Mw
6:1 ni kutoka nje ya maana yake halisi! Yuda alilenga “tukio la uasi wa
Shetani na malaika zake mbinguni ambao dhambi yao haikuwa mambo ya
zinaa za kibinadamu.
WANEFILI SIO UZAO WA NDOA ZA MALAIKA NA BINADAMU
Msamiati wa neno “wanefili uliotajwa kwenye Mw.6:4 halisemi ya kwamba
wamezaliwa kutokana na ndoa kati ya malaika na binti za wanadamu. Andiko
linasema: “Nao wanefili walikuwako duniani siku zile;….” Sio walizaliwa
wakati huo.
Pili, watoto waliozaliwa kwenye uasi huo imeandikwa
“…hao ndio watu hodari zamani, watu wenye sifa…” Hawa ni tofauti kabisa
na wanefili. Isitoshe yako maandiko mengine yanayotaja wanefili ambao
ni uzao wa binadamu na sio wa malaika (Hes.13:33)
MAJUMUISHO KWA SEHEMU YA KWANZA
Katika sehemu ya kwanza ya mada hii, nimejaribu kufafanua kwa kiasi
nilichojaliwa kuonyesha ya kwamba, “wana wa Mungu” ambao wametajwa
katika Mw.6:1-4 sio “malaika wa Mungu walioasi” kama ambavyo
imetafsiriwa na kuwaminiwa. Vigezo vya utetezi ni kutokuwepo kwa tafsiri
ya moja kwa moja kimaandiko kwamba “wana wa Mungu” hao walikuwa
“malaika wa Mungu.” Hoja ya msingi hapa ni hukumu ya Mungu ingelitolewa
kwa malaika walioasi badala ya binadamu.
Pili, Malaika kwa asili
hawana maumbile wala uwezo wa kuoa na kuzaa kama binadamu na viumbe hai
wengine duniani. Mbinguni hakuna kuoa wala kuzaana kama duniani(MT.22:)
Tatu, Maandiko yanasema waziwazi ya kwamba Mungu hajatoa hadhi wala
kutamka kwamba “malaika ni watoto wake”.
Mwisho ndoa
zilizofanyika hazijazalisha watoto wa kinefili na badala yake wanefili
wenye walikuwepo kabla na wakati ndoa hizo zinafanyika kwa wakati huo.
Sehemu ya pili inayofuata nitafafanua hao wana wa Mungu katika Mw.6:1-4
ni akina nani na ushahidi kamili wa maandiko yenye kuthibitisha
uchambuzi wangu. Kama umesoma ujumbe huu nijulishe kwa ku-like na
warushie na marafiki zako. NAKUTAKIA BARAKA ZA MWAKA MPYA 2017
Sign up here with your email
5 comments
Write commentsMh mie bado sijakuelewa vema mtumishi imeandikwa walivaa miili ya kibinadam wakafanya machukizo ili la kuvaa miili lipoje?? Na kuzaliwa majitu mbna hujazungumzia hayo majitu mtumishi
ReplyAksante sana kwa ufafanuzi juu ya jambo hilo! Ukipata Muda tafadhali, tufafanulie kuhusu "wana wa Mungu" wanaosemwa ktk Ayubu 2:1 ni kina nana! Kuzingatia kuwa yaliyosemwa ktk Mwanzo 6:1-4 hayana uhusiano na yalosema ktk Ayubu tajwa. Aksante mtumishi wa Mungu.
ReplyImeeleweka sana ubarikiwe ambao hawajalielewa ebu wakae watafiti pengine warudie kusoma wataelewa
ReplyHii ya pili nasubiri kwa hama , maana hapo ndio huwa nawaza kilasiku
ReplyAmina Mtumishi ubarikiwe sana, lakini malaika wanauwezo wa kuuvaa mwili na wakaishi kama binadamu je hili nalo umelifikiria. And then malaika walio hawako mbinguni
ReplyConversionConversion EmoticonEmoticon