SEHEMU YA MWISHO TAFSIRI KUHUSU WANA WA MUNGU NA BINTI ZA WANADAMU (MW.6:1-4)...

Bishop Sylvester Gamanywa
MAJUMUISHO
Mpendwa msomaji wangu, nimekwisha kuwasilisha mada hii ngumu ambayo nimechambua madai ya kambi kuu mbili za nadharia kuhusiana na maandiko ya Mw.6:1-4 ambapo maneno ya “wana wa Mungu”, “binti za wanadamu” na “wanefili” yamekuwa yakijadiliwa kwa miaka mingi. Aidha, uchambuzi wangu ulilenga kuelimisha kwa kuweka bayana madai ya dhana kuwa “wana wa Mungu” waliooa binti za wanadamu “sio malaika wa Mungu” na “wanefili” sio uzao wa “ndoa za malaika na binadamu.
Msingi wa uchambuzi wangu, hautokani na ushabiki wa kinadharia, bali ujuzi na uzoefu wangu katika kusoma, kutafiti na kutafsiri maandiko matakatifu kama yalivyoandikwa katika lugha za asili, na tafsiri za nakala mbali mbali za matoleo ya Biblia kwenye lugha nyinginezo.
Leo naomba nihitimishe mada hii kwa kuweka mkazo na msisitizo ulio bayana, bila kumun’gunya maneno ya kwamba, maandiko yote yanayotumika kutafsiri habari za “malaika wa Mungu kuoa binadamu na kuzaa nao” yamepotoshwa. Hapa nina maana na maandiko kuanzia: Mw.6:1-4; 2 Pet. 2:4; na Yud.1:14-15. Maana haya ndiyo yanayotafsiri isivyo sahihi kwa madai ya kuwa “malaika wa Mungu” kufanya ngono na binadamu na kuzaa nao watoto.
TAFSIRI ZA KUSHINIKIZA
Uchunguzi wa kimaandiko na tafsiri ya misamiati ya maneno yake umebaini kuwepo kwa tafsiri za kushinikiza ili kuhalalisha nadharia husika. Mathalan, tunaposoma katika Mwanzo: “Wana wa Mungu waliwaona binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wowote waliowachagua.” (Mw.6:2); hatuoni ya kwamba msamiati wa “wana wa Mungu” waliotajwa hapo walikuwa ni “malaika wa Mungu” waliojitwalia wake ambao ni binti za binadamu.
Tafsiri ya “malaika wa Mungu” ni kushinikiza. Ingelikuwa “wana wa Mungu” ni “malaika wa Mungu” kweli kweli; Musa mwandishi wa kitabu hicho angetaja moja kwa moja kuwa ni “malaika wa Mungu” waliofanya ngono na binti za wanadamu.
Narudia tena kusisitiza. Biblia katika Mw.6:2 haijataja wala haijasema, ya kuwa “wana wa Mungu” walikuwa ni “malaika wa Mungu”. Kama Biblia haijasema moja kwa moja na waziwazi jambo husika, ni dhahiri kwamba "neno tunalopachika" hapo tunalazimisha kupata maana tunayoitaka sisi; lakini kweli ya neno lenyewe itabaki vile vile kwa kila mwenye kutafuta kuijua kweli ya andiko husika
Pili, hata baadhi ya maandiko ya Agano Jipya yanayo tafsiriwa ya kwamba "uasi wa malaika" ulikuwa ni wa “ndoa za malaika na binadamu” sio kwamba ni tafsiri ya kushinikiza tu bali pia ni tafsiri potofu. Mathalan, Petro alipoandika: “Kwa maana ikiwa Mungu hakuwaachilia malaika waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe hata ije hukumu;..” (2 Pet.2:4) Vigezo vya kutafsiri maandiko matakatifu juu ya msamiati wa “malaika waliokosa” havioneshi wala kuleta maana ya kwamba “makosa yao” yalikuwa ni “ndoa za malaika na binadamu”.
Hata maandiko ya Yuda yasemayo: “Na malaika wasioilinda enzi yao wenyewe, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu, amewaweka katika vifungo vya milele chini ya giza kwa hukumu ya siku ile kuu.” (Yud.1:6) Ukichunguza kwa makini msamiati wa “malaika wasioilinda enzi yao, lakini wakayaacha makao yao yaliyowahusu” utaona ya kuwa hausemi wala hauleti maana ya “malaika kuacha enzi yao na makao yao” ati ni “kujitwalia wake za binadamu na kuzaa nao”.
TAFSIRI YA YESU KRISTO KUHUSU MALAIKA
Tamko la Yesu Kristo kuhusu malaika linajibu maswali yote yenye utata wa dhana kuhusu “malaika kuoa binadamu na kuzaa naye”. Malaika hawahitaji na hawawezi “kuoa wala kuzaa watoto” wawe wa kimalaika au kibinadamu. Maana hawakuumbwa katika mfumo wa kuzaliwa kukua na kufa. Hawafi wala hawapungui na wala hawaongezeki. Tunapata ushahidi wa kimaandiko kama ifuatavyo:
“Kwa maana katika kiyama, hawaoi wala hawaloewi, bali huwa kama malaika mbinguni.” (MT.22:30) “Kwa maana watakapofufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, bali huwaa kama malaika walioko mbinguni.” (MK.12:25) “Wala hawewezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo.” Luk.20:36)
Ni muhimu kuzingatia ya kuwa aliyesema haya maneno ni Yesu ambaye asili yake ni kutoka Mbinguni; na ndiye aliyeuwaumba hao malaika: “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika.” (YH.1:3) Unaona? Yesu aliposema “malaika hawaoi” yeye mwenyewe ndiye aliyewaumba na anajua kwamba hawana asili wa uwezo au mamlaka ya kuvaa miili ya binadamu ya kuoa na kuzaa na binadamu.
Kana kwamba hii haitoshi, Yesu Kristo katika mafundisho yake, hakuwahi kutaja ya kuwa “uasi wa malaika” ulikuwa ni “mwingiliano wa kindoa na binadamu.” Badala yake tunasoma Yesu akitaja habari za asili ya uasi wa Ibilisi pale aliposema: “Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye ni mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (YH.8:44)
Unaona? Kama uasi wa Ibilisi ungelikuwa ni “mwingiliano wa kingono na binadamu” kamwe Yesu asingeacha kuusema ukweli huo. Lakini hapa tunasoma akimwita shetani kuwa ni “Mwuaji” na “baba wa uongo” lakini sio “baba wa ndoa za malaika na binadamu.”!
UTATA WA KUWEPO KWA “MAJINI MAHABA”
KUFANYA NGONO NA BINADAMU
Yesu alitoa mfano halisi ya kwamba pepo mchafu anaweza kuugeuza mwili wa mtu kuwa nyumba yake. Na akitolewa huondoka lakini akikosa mahali pa kukaa huamua kurudi:
“Halafu husema, nitarudi nyumbani kwangu nilikotoka; hata akija, aiona tupu, imefagiwa, na kupambwa. Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko kwanza….” (MT.12:44-45)
Kwa maandiko tuliyosoma, tunajifunza yafuatayo: 1. Pepo wachafu wana uwezo wa kuingia katika mwili wa binadamu na kukaa ndani yake. 2. Pepo akiwa ndani ya mwili wa binadamu ana uwezo wa kuathiri akili, hisia na utashi wa binadamu. 3. Pepo mchafu akiwa ndani ya mwili wa binadamu ana uwezo wa kuchochea tamaa za binadamu kufanya vitendo vya ngono kinyume na maadili ya ndoa.
Mambo ambayo yanatafsiriwa isivyo sahihi kuhusiana na pepo wachafu ni kama ifuatavyo: 1. Madai juu ya pepo kujifanyia miili ya kibinadamu ili wapate kufanya ngono na binadamu. 2. Kuna tofauti kati ya kupagawa na pepo akatumia mwili wa binadamu kufanya ngono na binadamu. Lakini pepo mwenyewe hawezi kufanya ngono na binadamu kimwili.
Madai ya kwamba watu wanaolewa au kuoa majini na kuzaa nao sio sahihi. Kinachofanyika kwa wenye madai haya ni “hali ya kupagawa na majini ambayo yamo ndani ya miili yao na kuwasumbua kimawazo na kisaikolojia kuhusu ngono” lakini sio kwamba ni tendo halisi la ngono linalofanyika. Hata wenye kudai kuzaa na majini huwezi kuwaona hao watoto kwa sababu kimsingi huwa ni viini macho na mazingaombwe tu. Na hii ndiyo maana ya Yesu kusema “Shetani ni mwongo na baba wa huo.” (YH.8:44)
UTATA WA CHANZO CHA NADHARIA
YA NDOA ZA MALAIKA NA BINADAMU
Utafiti wa kihistoria kuhusu Nadharia ya "malaika waliasi kwa kuvaa miili ya binadamu na kuoa na kuzaa na binti za wanadamu" umegundua chanzo chake ni "Kitabu cha Henoko" ambacho hakitambuliwi kuwa ni "maandiko matakatifu yaliyovuviwa na Mungu"!
Kitabu hicho cha Henoko ndicho kimeandika moja kwa moja kikidai: "Malaika wa Mungu mbinguni waliwatazama binti za wanadamu duniani, wakawaona wanavutia kwa tendo la ngono wakaacha enzi yao wakashuka duniani, wakaamua (kuoana) na binti za wanadamu na kisha wazaa nao watoto wa kinefili-wanefili ambao ni majitu."
Kitabu hicho kilisomwa hata na baadhi ya wakristo maarufu wa karne za kwanza walivutwa na taarifa zake baadhi yao wakiwemo akina Tertullian, Irenaeus, Origen, na Clement wa Alexandria. Lakini baadaye Kitabu cha Henoko kilikataliwa kuingizwa kwenye orodha ya maandiko matakatifu ya Agano la Kale. Mojawapo ya sababu ya kukataliwa ni japokuwa kimetajwa kuwa ni kitabu cha Henoko lakini hakikuandikwa na Henoko mwenyewe.
Nakushukuru kwa kufuatana nami katika mada hii ngumu na tata. Kama umeguswa na mada hii nitakushukuru kama uta-like na kuwajulisha marafiki zako wengine. Tukutane katika mada mpya ijayo. Ubarikiwe sana katika mwaka huu mpya wa 2017.
Previous
Next Post »