"UPAKO WA KUFANYA ZAIDI YA WENGINE"

Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila
"Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, Yesu wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, Yesu, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi unirehemu. Yesu akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, Bwana, nipate kuona. Yesu akamwambia, Upewe kuona; Imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza Mungu. Na watu walipoona hayo walimsifu Mungu. " (Luka 18:35-43).
Mambo ya kujifunza;
1. "Mabadiliko yoyote unayoyataka yanaanza na wewe."
Huyu ndugu alikuwa akiisha kwa kuombaomba. Alikuwa ni mtu aliyezoeleka na kutambulika kwa "kazi yake" ya kuombaomba.
Alipotaka mabadiliko, kutoka hapo alipo kwenda anapotaka, hakuhitaji mtu mwingine aje na kumsukuma au kumbadilisha bali alichukua hatua ya kwanza kuyaelekea mabadiliko anayoyataka, na katika mchakato huo ndipo muujiza wa mabadiliko ukatokea.
Unawakumbuka wale wakoma watatu enzi za nabii Elisha? Hakuna kilichobadilika maishani mwao mpaka walipochukua hatua ya kwanza kuyaendea mabadiliko wanayotaka bila kujali hatari ya kuuwawa na Washami(risk taking), na walipotenda sehemu yao, Mungu akathibitisha muujiza wao.
Kama huyu ndugu kipofu angelikaa kimya asingeliponywa.
Kama mwanamke Msoforonike aliyekuwa na mtoto aliyeteswa na pepo kwa muda mrefu asingelichukua hatua ya kuanza kuchukua hatua kuyaelekea mabadiliko anayotaka juu ya mwanae, mtoto yule angeliuwawa na yale mapepo huku anaona!
Change is you... Whatever you can imagine, Whatever you can see, If you will only take a step of faith out of comfort zone you will become and you will achieve..!
Tabia ya Mungu ni kuziongoza hatua za mtu pale mtu anapochukua hatua ya imani kuthubutu kutoka alipo kwenda "anapoona moyoni mwake" kwamba anaweza kufika au kuwa (Mithali 16:1,9).
2. "Unapopita kwenye changamoto, ugumu au tatizo lolote, mbali ya kuomba, hakikisha umefumbua macho yako ya rohoni na masikio yako ya rohoni na mwilini kupokea jibu lako"
Huyu ndugu alikuwa amekusudia tayari kugeuka, alikuwa tayari kutoka alipo kwenda kule anakotamani kuwa, Lakini alihitaji "ishara" kujua ya kuwa muda wa mabadiliko na muujiza wake umefika.
Na ili kujua hili hakuomba tu moyoni na kufunga masikio yake, bali alihakikisha "anafuatilia na kupata taarifa sahihi" zinazohusu anachokitaka.
Kijana wa kike au wa kiume unataka kuoa au kuolewa, na umeomba kwa Mungu tayari lakini umeishia hapo tu, hutafuti maarifa, hekima na ufahamu wa Kimungu wa namna ya kumtambua mwenzi wako kati ya wengi watakaopita maishani mwako mara tu baada ya maombi.
Mwingine unaomba Mungu akusaidie akupe neema upate kazi lakini huna taarifa zozote kuhusu soko la ajira, hujui hata kuandika CV, huna communication skills nzuri, hujaanza kujijengea tabia na mfumo wa maisha kama wa mtu anayesubiri kuwa kwenye ajira muda wowote, Fursa ikija waliojiandaa wataipata na utaishia kusambaza bahasha tu!
Ndivyo ilivyo kwa kila kitu kinachohusu maisha.
Biblia inasema, "bahati na wakati (time and chance)" huwa vinamtokea kila mtu lakini ni wale "waliokuwa macho" na "waliokuwa wametega masikio" ndio watakaoweza kuzifaidi!
Walikuwepo vipofu wengi kipindi hicho lakini huyu ndugu pekee ndiye aliyesaidika kwa sababu "alikuwa makini" kusikia na "kupata taarifa" sahihi za kumhamisha hapo alipo.
Walikuweko wakoma wengi enzi za nabii Elisha lakini ni Naamani Mshami tu aliyefaidika na upako uliokuwa juu ya Elisha.
Kulikuwa na wanawake wengi waliokuwa "wakitokwa na damu (magonjwa ya uzazi na mfumo wa uzazi kwa ujumla)" lakini ni yule tu "aliyekuwa ametega sikio" na kusikia taarifa sahihi kuhusu Yesu ndiye aliyeponywa kwa pindo la vazi ambalo wengine waliligusa kimazoea, bila ufunuo na wakabaki na misiba yao!
Be informed... Go for right information about anything you real want to do or become... The Bible instruct us "to pray and watch" not praying only!
3. "Uwe makini na waliotangulia"
Biblia inasema, "Basi wale waliomtangulia... Wakamkemea ili anyamaze..."
Hiki ni kitu cha ajabu sana. Watu "waliotutangulia" mara zote ndio hutuzuia au kutukatisha tamaa.
Huyu ndugu aliwaendea "waliotangulia" lakini haohao ndio walitaka "kunyamazisha na kuzima kabisa maono yake"... Watu wengi wamekata tamaa na kuvunjika moyo kwa sababu ya "waliowatangulia"...
Kuna wengine wanaogopa kuoa na kuolewa kwa sababu "waliotangulia" kwenye taasisi ya ndoa "wamekwama" kudhihirisha kwamba "ndoa ni paradiso ndogo" badala yake imekuwa "ndoa ndoano" kiasi kwamba wale "walio nje" wanaogopa kuingia kwa sababu "waliotangulia" wamewaambia maneno mazito na magumu au wameona yanayowakuta hao "waliotangulia" kwenye ndoa zao!
Kuna wengine "wenye huduma" za ajabu sana, lakini wamekwama kuwa kama vile "walivyokuwa wakijiona" kwa sababu "waliowatangulia" waliwavunja moyo au kuwajeruhi.
Kuna watu wameogopa kuacha kazi za kuajiriwa na kujitegemea/ kuanzisha biashara zao kwa sababu "waliotangulia" wamewaambia wanajihatarisha, bora wakae kwenye ajira maana kuna security!
Unapoongea na waliotangulia hakikisha unaongea na watu wanaoamini katika kuwezekana, mashujaa wa imani na watu waliothubutu na kufanikiwa katika maono yao!
Waliotangulia ni wa muhimu kwa sababu wana uzoefu lakini usikubali "wakanyamazisha" kile ulichokibeba na unachokiona ndani.
Usifikiri mtu wa kwanza kubuni na kutengeneza "simu ya mkononi isiyotumia waya" alikubaliwa wazo lake na "waliotangulia" kutengeneza simu za waya... Lakini ashukuriwe Mungu kwamba hakukubali wazo lake linyamazishwe, na leo tunazo simu za mkononi na si za waya tena!
Kilichomsaidia huyu kipofu ni "kuzidi kupaza sauti" yaani kuzidi kuyaamini na kuyaatamia maono yake bila kujali "waliotangulia" wanasemaje!
Hivi ndivyo unavyopaswa kuwa... Mtu awaye yote asikudharau na kukwambia eti huwezi kufanya hicho ambacho moyoni mwako wewe "unakiona" na unaamini kabisa kinawezekana!
Hiki ndicho chakula cha washindi leo,
Umebarikiwa,
Mwl D.C.K
Previous
Next Post »