Katika sehemu ya kwanza, nilitambulisha kambi
mbili kuu za nadharia zinazokinzana kuhusu “wana wa Mungu” walioatajwa
katika Mw.6:1-4 ni akina nani. Kambi moja inafundisha ni “malaika wa
Mungu” walioasi kwa kuoana na binadamu na kuzaa watoto wa kinefili.
Kambi ya pili inafundisha “wana wa Mungu” ni uzao wa Sethi” ambao
walikengeuka na kuoana na binti za wanadamu wa “ukoo wa Kaini.”
Katika uchambuzi wa awali nilipingana na “nadharia ya malaika kuoana na
binadamu”. Leo nawasilisha uchambuzi wa unaoangukia katika tafsiri ya
pili inayofundisha kwamba “wana wa Mungu” sio malaika bali ni binadamu.
Nitaanza kwa kuelezea chimbuko la historia ya ukoo wa uzao wa nyoka;
pili chimbuko la historia ya ukoo wa “wana wa Mungu”, na tatu
nitachambua kuhusu Mkengeuko Wa Maadili Ya Ndoa Kwa “Wana Wa Mungu”
Kuoana Na Wasioamini. Karibuni:
1. Chimbuko La Historia Ya Ukoo Wa “Uzao Wa Nyoka”
Katika Mw.3:15 tunasoma ya kuwa Mungu mwenyewe ndiye alitabiri aina 2
tofauti za uzao pale alipotaja kuhusu “uadui” kati ya Uzao wa nyoka" na
"uzao wa Mwanamke" (MW.3:15) Kutokana na “tamko la uadui” likawa ndilo
chimbuko la “wana wa Mungu” na “binti za wanadamu” katika Mw.6:1-4.
Tukisoma katika Mwanzo Sura za 4 na 5 tunakuta ushahidi wa kihistoria
ya watoto wa kwanza kiume wa Adamu, Kaini na Habili. Humo tunashuhudia
jinsi ambavyo: “BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; lakini Kaini
hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake
ukakunjamana.” (Mw.4:4b-5) Baadaye tunamsoma Kaini anamwua Habili mdogo
wake na kulaaniwa na Mungu: “Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi,
iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;…”
(Mw.4:11) Kuanzia hapo Kaini akawa ndio mwasisi wa “uzao wa nyoka”!
Kwa kupitia uzao wa Kaini tupata orodha ya watoto wake kuanzia Henoko,
Iradi, Mehuyaeli, Methushaeli ambaye alimzaa Lameki. (Mw.17-18) Ni
kwenye “ukoo wa uzao wa nyoka (Kaini) tunamkuta Lameki akianzisha
utaratibu wa “ndoa za wake wengi”, kinyume cha maadili ya ndoa ya mke
mmoja tangu Adamu na Hawa. (Mw.4:19)
Ushahidi mwingine
unaothibitisha ya kuwa Kaini ndio “uzao wa nyoka uliolaaniwa”, ni pale
mjukuu wake Lameki alipotoa kiapo hasi cha kuendeleza visasi vya mauaji
kama babu yake: “ ….enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; maana
nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; kijana kwa kunichubua; kama Kaini
akilipiwa kisasi mara saba, hakika Lameki atalipiwa kisasi mara sabini
na saba.” (Mw.4:23-24)
2. Chimbuko La Historia Ya Ukoo Wa “Wana Wa Mungu”
Baada ya ukoo wa “uzao wa nyoka” kupitia Kaini kuongezeka, tunamkuta
Adamu amepata mtoto mwingine wa kiume akamwita jina lake Sethi. Sethi
naye akamzaa Enoshi ambapo tusoma ya kuwa ndipo watu walipoanza kuliitia
jina la BWANA.” (Mw.4:25-26)
Kwa mantiki hii, Sethi akawa ndiye
baba wa ukoo wa “wana wa Mungu”! Ukoo wenyewe umeanishwa kwa kirefu
katika Mwanzo 5:5-32 ukianzia kwa Sethi, Enoshi, Kenani, Mahalaleli,
Yaredi, Henoko, Methusela, Lameki (si yule wa Kaini).
Ushahidi
mwingine unaothibitisha ya kuwa “wana wa Mungu” ni “uzao wa Sethi” ni
Nuhu ambaye ndiye aliyeonekana mtu wa haki wa kuendeleza ukoo safi wa
wana wa Mungu baada ya hukumu ya Gharika: “Nuhu akapata neema machoni pa
BWANA….Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu
alikwenda pamoja na Mungu.”(Mw.6:8-9)
3. Mkengeuko Wa Maadili Ya Ndoa Kwa “Wana Wa Mungu” Kuoana Na Wasioamini
Sasa tuje kwenye kiini cha mjadala wa kisa cha Mw.6:1-4. Ushahidi wa
kimaandiko katika kisa hiki unaonesha chimbuko la uharibifu sio “ndoa za
malaika na binadamu” kama ilivyo kwa mtazamo wa nadharia husika.
Kiini cha mgogoro hapa ni “mkengeuko wa maadili ya ndoa” uliosababishwa
na “Ukoo wa Sethi” ambao ndio “wana wa Mungu’ kuoana na binti za ukoo
wa Kaini ambao hawakupaswa kuchangamana kifamilia. Mungu alikasirishwa
na ukengeufu huu wa wana wa Sethi kuamua “kujitwalia wake waliowataka”
kutoka ukoo wa Kaini na kuzaa nao watoto. Lakini sio hilo tu bali
walivuka mipaka kwa kuacha utaratibu ndoa ya mke mmoja kwenda ndoa za
wake wengi: “wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni
wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua.” (Mw.6:2)
Msamiati wa neno “kujitwalia wake" kwa kiebrania ni laqah ukimaanisha
“muungano wa kindoa” au “kujipatia mke”. Msamiati huo huo umetumika pia
kwa “kujitwalia wake” kwa njia ya kuvunja maadili ya kimungu ya ndoa ya
mke mmoja(Mw.2:23-24;MT.19:4-5) kwenda “ndoa za wake wengi” kama
alivyofanya mjukuu wa Kaini:
“Lameki akajitwalia wake wawili,
jina la kwa kwanza ni Ada, na jina la pili ni Sila.” (Mw.4:19) Hii ndiyo
iliyomkasirisha Mungu kiasi cha kufupisha “kiwango cha ukomo wa
kuishi”(Mw.6:3) duniani; na kisha kufutilia mbali kizazi chote cha
binadamu na viumbe hai wote dunia nzima. (Mw.6:5-7)
Mpango wa
Mungu tangu mwanzo ni kutunza ukoo safi wa uzao wa mwanamke ambao
ungemzaa Yesu Kristo awe mkombozi wa ulimwengu. Ibilisi akamponda “adamu
kisigino cha uasi” kwa kumwingia mzaliwa wa kwanza Kaini akalaaniwa.
Ukoo wa Sethi ndio uliotegemewa kumleta mkombozi lakini nao pia
ukaingiliwa na kukengeuka. Kwa neema akapatikana Nuhu na uzao wake.
Hata baada ya gharika tunaona Mungu aliendeleza msimamo wake mkali kwa
“wana wa Mungu” wa kutokuingiliana kindoa na mataifa yenye kuamini
miungu mingine: “Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda
kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja
akakuita ukaila sadaka yake. Ukawaoza wana wako binti zao, na binti zao
wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakavuta wana wenu wafanye uzinzi
na miungu yao.” (Kut.34:15-16)
“…..usifanye agano nao, wala
kuwahurumia, wala usioane nao; binti yako usimpe mwanawe mume, na wala
usimtwalie mwano mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume
asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira
ya BWANA juu yenu, naye atakuangamiza upesi..” (Kumb.7:2-4)
UFAFANUZI WA NYONGEZA KUHUSU
NDOA ZA MALAIKA NA BINADAMU
NDOA ZA MALAIKA NA BINADAMU
Kwenye makala iliyopita, baadhi ya wasomaji ninaowaheshimu sana
waliuliza maswali kuhusu uhalali wa maelezo yangu ya kutokukubaliana na
nadharia ya “wana wa Mungu” kuwa sio malaika. Walitaka kujua msamiati wa
kiebrania wa “wana wa Mungu” unasemaje kama hauna maana ya malaika wa
Mungu kuwa ndio wana wa Mungu. Na wengine wametaka kujua chimbuko la
wanefili.
Naomba kuongeza ufafanuzi wa nyongeza katika kujibu
maswali yaliyokwisha kuulizwa kama ifuatavyo: Tafsiri ya kiebrania ya
“wana wa Mungu” ni bene ha'elohim. Katika Agano la Kale msamiati huu
unapatikana sehemu kuu mbili kwenye Agano la kale. Ayu 6:1 na Ayub 2:1.
Kwenye Ayu38:7 neno “ha” halipo. Katika sehemu hizo mbili tafsiri ya
bene ha’elohim (wana wa Mungu) lilitumika kwa kwa malaika na mahali
pengine kwa binadamu pia. (Hos.2:1; Kumb.14:1)
Lakini
ukiuchunguza kwa makini muktadha wa maandiko ya kitabu cha Mwanzo
utakuta hakuna mahali popote ambapo nadharia hii ya “wana wa Mungu” kuwa
ni “malaika wa Mungu” imetajwa. Iwe ni katika Mwanzo au katika vitabu
vyote vya Musa vya Kutoka, Hesabu, Walawi, na Kumbukumbu la Torati. Kwa
maelezo mengine hii ni tafsiri ya kuazima kutoka kwenye vyanzo vingine
ambavyo matumizi ya misamiati yake nayo haina uhusiano na tukio la ndoa
zinazodaiwa kuwa za malaika na binadamu katika Mw.6:1-4)
Kana
kwamba hii haikutosha, kuna uthibitisho wa kitafiti kwamba nadharia ya
“malaika kuoana na binadamu” ilipata nguvu zaidi kutoka chanzo kingine
cha taarifa cha “Kitabu cha Henoko” ambacho ndicho kimesimulia habari za
ndoa za malaika kuacha enzi yao na kujitwalia wake za kibinandamu na
kuzalisha watoto wa kinefili. Kitabu hicho kilitumiwa sana na baadhi ya
wakristo maarufu wa karne za kwanza waliovutwa na taarifa zake wakiwemo
akina Tertullian, Irenaeus, Origen, na Clement wa Alexandria.
Lakini baadaye Kitabu cha Henoko kilikataliwa kuingizwa kwenye orodha ya
maandiko matakatifu ya Agano la Kale. Mojawapo ya sababu za kukataliwa
ni paamoja na ukweli kwamba kitabu cha Henoko hakikuandikwa na Henoko
mwenyewe. Hata hivyo baadhi ya wanazuoni wa tafsiri ya maandiko ya Kale
waliendelea kutumia nukuu za kitabu hicho katika kutafsiri maandiko
matakatifu.
CHUMBUKO LA WANEFILI
Watu wengi wameuliza
maswali kuhusu wanefili ni akina nani na walitokea wapi! Katika sehemu
ya kwanza nilijibu kwa sehemu ya kwamba, wanefili sio uzao wa
kinachodaiwa ni mwingiliano wa kingono kati ya malaika na binadamu.
Jina la “wanefili” hali maana moja ya “majitu”. Pia kuna maneno tofauti
ya kiebrania yenye tafsiri ya Wanefili. Kuna neno “naphal”
likimaanisha “kuwashukia wengine” au “wenye kushambulia wengine” katika
Yos 11:7; Ayu.1:15 na Yer.46:16. Neno la pili ni “palah” likiwa na
maana “watu wasio wa kawaida” (extraordinary) Hii inamtaja mfalme mwenye
nguvu nyingi mno za kuharibu kiasi cha kustaajabisha watu…(Dan.8:23-24)
Lakini pia wanefili lilitumika kwa binadamu wenye maumbile
makubwa kama Goliati (1 Sa.17:4; 21:19-20) Sehemu nyingine ambapo
tunasoma habari za wanefili ni wana wa Anaki katika Hes.13:22,28,33).
Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa chimbuko la wanefili sio uzao wa ndoa
za malaika na binadamu. Ni jamii ya watu waliotokana na uzao wa
binadamu. Sasa kama hawa wanefili wa Wana wa Anaki walizaliwa na
binadamu aliyeitwa Anaki, hali kadhalika na wanefili wa Mw 6:4. Nao
walizaliwa na wana wa ukoo wa Kaini, na hasa kwa tabia yao ya ukatili wa
kushambulia binadamu wengine katika jamii za wakati huo.
Pia
kuna tofauti kati ya “wanefili” na “wana wa waliozaliwa kutokana na ndoa
haramu za kibinadamu ambao wanaitwa “watu waliokuwa hodari na wenye
sifa.”
Najua ya kwamba uchambuzi huu ni mgumu kwa baadhi.
Nitakuwa tayari kujibu maswali yoyote yatakayoulizwa kutoka na uchambuzi
wangu. Nitafurahi pia kupata maoni yako. Ubarikiwe sana.
Sign up here with your email
2 comments
Write commentsNaitwa Joseph Maziku, nimefurahiswa sana na ufafanuzi wako kuhusu chimbuko la wanefili
ReplyLakini Nina swali moja kuhusu gharika
Mungu alipowaangamiza wanadamu na kumbakiza Nuhu na familia yake tena Ni familia inayo mwamini yeye JEHOVA, Je kulikuwa na haja gani YEHOVA kuwaonya wasioane na watu wa mataifa wakati kipindi hicho hapakuwa na watu wakenguufu maana wote waliteketea katika gharika kuu, je hao watu wa mataifa na wanaoabudu miungu wengine walitoka wapi?
Samahani nakujibu,,,, lengo la Mungu lilikuwa ni kupata familia, ukoo, kabila,,Taifa la Mungu ambao Yesu angezaliwa kupitia mlolongo huo, sasa baada ya kuchagua Ibrahim,alimwonya wazao wake wasioe oe Bila utaratibu, waoe sehemu sahihi
ReplyConversionConversion EmoticonEmoticon