kuhusu kunyakuliwa kwa kanisa la Kristo.
Bishop sylvester Gamanywa |
Mada hii
inaanza kwa kuchambua maana ya misamiati wa kunyakuliwa, jinsi tukio
litakavyokuwa, sababu za kunyakuliwa; na mchakato wa maandalizi ya
unyakuo wenyewe. Karibuni.
MAANA YA KUNYAKULIWA
"Kunyakuliwa" ni tukio maalum la kinabii ambalo linatarajiwa kutokea
wakati wowote kwa ajili ya kuhitimisha huduma za Kanisa la Kristo
duniani. Tukio hili linawahusu makundi mawili ya walengwa. Kundi la
kwanza ni “kufufuliwa kwa wafu waliolala mauti katika Kristo”! Na kundi
la pili ni “wanafunzi halisi wa Yesu Kristo tutakaokutwa hai. Na hii ni
kwa mujibu wa maandiko ya Paulo alipowaandikia Wathesalonike:
"Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije
mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. Maana, ikiwa twaamini ya
kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika
Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno
la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake
Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. Kwa sababu
Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya
malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo
watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa
pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa
pamoja na Bwana milele. Basi, farijianeni kwa maneno hayo." (1 THE.
4:13-18)
JINSI UNYAKUO UTAKAVYOFANYIKA
Tukio hili la
kinabii litafanyika kwa kasi na kwa kushtukiza. Hakutakuwepo na taarifa
ya kujiandaa kwa unyakuo. Maandiko yanasema kwamba itakuwa ni: "kwa
dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana
parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi
tutabadilika." (1 KOR. 15:52)
Kwa sababu ya kushtukiza kwa tukio
hili la ghafla imeandikwa ya kuwa kuna baadhi waliotakiwa kunyakuliwa
wataachwa kwa sababu ni kwa ajili ya watakaokutwa wako tayari tu ndio
watakaonyakuliwa:
"Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu,
ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Kwa kuwa kama vile siku
zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa,
wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa
kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni;
mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja
atwaliwa, mmoja aachwa.Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi
atakayokuja Bwana wenu." (MT. 24:37-42)
SABABU ZA KUNYAKULIWA
Baada ya kupitia tafsiri na jinsi unyakuo utakavyofanyika, napenda
tupitie hoja muhimu za sababu za kunyakuliwa. Napenda kuzielezea sababu
hizi kwa sababu kuna malumbano ya kitheolojia kuhusu unyakuo na mjadala
ukilenga ni wakati gani unyakuo utafanyika.
Kuna kundi lenye
kudai kunyakuliwa kutafanyika kabla kuanza kipindi cha miaka 7 ya dhidi
kuu (Pre-tri-rapture) ; kundi la pili linaamini unyakuo utafanyika
katikati ya kipindi cha miaka 7(Mid-tri-rapture); na kundi jingine
linaamini kunyakuliwa kutafanyika mwishoni mwa dhiki kuu
(Post-tri-rapture)
Uchunguzi wangu na imani yangu vinaangukia
katika kundi la kwanza la(Pre-tri-rapture) na ndiyo maana nimeona nitoe
sababu za kunyakuliwa kabla ya kuanza kipindi cha dhiki kuu.
1. Ahadi ya Yesu Kristo
Yesu mwenyewe ndiye aliyetangulia kuwajulisha wanafunzi wake kuhusu
suala la kurudi tena kuwachukua ili wakae pamoja naye mbinguni: "
Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia;
maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia
mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi
mwepo." (YN. 14:2-3)
2. Kuepushwa na ghadhabu ya Mungu
Mtume Paulo alidokeza habari za ujio wa Mpinga Kristo na atakavyotawala
chini ya uvuvio wa Shetani mwenyewe. Na Kisha akataja habari za wale
watakaochwa baada ya unyakuo watakavyoingia kwenye kipindi cha
udanganyifu mkubwa wa Shetani kwa sababu walikataa kuamini kweli ya
Injili kabla ya unyakuo:
“Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi,
ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa
ufunuo wa kuwapo kwake; yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda
kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo; na katika
madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali
kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa. Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya
upotevu, wauamini uongo; ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli,
bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.” (2 THE. 2:8-12)
Kwa hiyo, kunyakuliwa kabla ya kipindi cha utawala wa MpingaKristo ni
ili tuepushwe na hii ghadhabu ya Mungu inayotarajiwa kuupata ulimwengu
katika kipindi hicho: “Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu,
jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia Mungu
mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai, wa kweli; na kumngojea
Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni Yesu,
mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja.” (1 THE. 1:9-10)
TISHIO LA KUACHWA KAMA HAKUNA MAANDALIZI
Kufuatia tukio la kunyakuliwa kufanyika ghafla, ndiyo maana maandiko
yanahimiza walengwa wa unyakuo kuwa tayari wakati wote ili wasijekuachwa
wakati wa unyakuo. Na hii ndiyo sababu ya kuamini kwamba unyakuo
utafanyika kabla ya kipindi cha dhiki kuu ili walengwa wawe wametimiza
vigezo vya unyakuo huo wasijepatwa na mabalaa ya dhiki kuu.
Ushahidi ni maandiko yanayo tahadharisha kuwa tayari, kutubu na kuishi
maisha ya utakaso kamili wakati wote: "Na ndani yake hakitaingia kamwe
cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali
wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo." (UFU.
21:27)
Yesu mwenyewe aliyaonya makanisa ya Karne ya kwanza
yajitakase na kujiweka tayari kwa unyakuo vinginevyo yatakosa fursa
hiyo. Kwa Kanisa la Efeso alilionya akisema: "Basi, kumbuka ni wapi
ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya
hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake,
usipotubu." (UFU. 2:5)
Maana ya "Kuondolewa kinara" ni kufutiwa
haki ya urithi wa ufalme wa mbinguni na kufutwa jina kwenye kitabu cha
uzima. Mtume Paulo naye anasisitiza akisema kwa kuwa siku ya unyakuo
yaja kama mwivi na itawakumba wote wasiojiandaa;akasema sisi tusikubali
kubaki gizani mpaka tuvamiwe ghafla:
“Maana ninyi wenyewe mnajua
yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku. Wakati
wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula,
kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. Bali
ninyi, ndugu, hammo gizani, hata siku ile iwapate kama mwivi.” (1 THE.
5:2-4)
Tutaendelea na sehemu ya pili ambapo tutapitia mchakato wa
maandalizi kwa ajili ya kunyakuliwa, ni mambo gani yatakayojiri baada
ya unyakuo mbinguni na nini kitaendelea duniani. Tafadhali kama ujumbe
huu umekugusa nijulishe kwa ku-like ukurasa huu na kisha warushie na
marafiki zako wengine.
Sign up here with your email
1 comments:
Write commentsasante sana
ReplyConversionConversion EmoticonEmoticon