Bishop Sylvester Gamanywa |
KAMBI YA UNYAKUO KABLA YA DHIKI KUU
UNYAKUO KABLA (PRE-TRI) ni kambi ya nadharia inayofundisha ya kwamba kunyakuliwa kutafanyika KABLA ya kuanza kwa kipindi cha dhiki kuu. (Yh.14:1-4; 2 Thes.2:7-12).
Aidha, kambi hii inasimamia maandiko ya: "Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa. Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake..." (2 Thes.2:7-8)
Kambi hii inatetea msimamo wake kutokana na maneno ya Yesu aliyoliahidi kanisa la Thiatira kwamba ataliepusha lisiingie kwenye kipindi cha dhiki kuu (Ufu.3:10)
Kambi hii pia inayatafsiri maneno ya Yesu katika Injili ya Mathayo Sura ya 24 kuwa ni maonyo ya kinabii kwa ajili ya taifa la Israeli na majanga yatakayowapa wakati wa dhiki kuu na sio kwa kanisa
KAMBI YA UNYAKUO KATIKATI MWA DHIKI KUU
Kambi hii yenyewe imeamua kusimama katikati na kufundisha ya kuwa Kanisa lazima lipitie katika dhiki: (Matt. 5:11-12, 10:34-35, 24:1-31; Mk.13:1-27; Lk 21:1-28; Yh 16:33, 17:15; Yk1:2-15; 1 Pet. 4:12-19).
Kambi hii ya unyakuo kufanyika katikati mwa dhiki kuu ni utetezi kwamba Kanisa halitashiriki mapigo ya ghadhabu ya Mungu (Lk 21:36). Kwa hiyo Kanisa litanyakuliwa katikati ya dhiki kuu ili kuepushwa ghadhabu ya Mungu katika dhiki kuu ((Rum. 5:9; 1 Thes. 1:10, 5:9)
KAMBI YA UNYAKUO BAADA YA DHIKI KUU
Kambi hii ni kongwe na inafundisha ya kwamba Kanisa litakuwepo katika dhiki kuu na kunyakuliwa mwishoni mwa dhiki kuu ((Matt. 24:29-31)
Msimamo wa kambi hii unasimamia nukuu za maandiko yasemayo: “Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu yeyote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo.” (MT.24: 21-22)
Kisha wanasimamia nukuu za maneno ya “Lakini mara , baada ya dhiki ya siku zile……..ndipo itakapoonekana ishara yake Mwana wa Adamu mbinguni……nao watamwona Mwana wa Adamu akija juu ya mawingu ya mbinguni pamoja na nguvu na utukufu mwingi…… Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu.” (MT. 24:29-31)
Kisha wanatumia nukuu za maneno yasemayo:“…Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule.” (MT. 24:24)
Kwa mtazamo wa kambi hii msamiati wa neno “wateule” unatafsiriwa kuwa ni “kanisa”! Wanafundisha ya kwamba: i) Kanisa litakuwepo duniani kwa kipindi chote cha dhiki ya siku za mwisho, ii) Kanisa litakutana na upinzani wa Mpingakristo na chapa yake ya mnyama, iii) Kila mtu duniani, wakiwemo wote wanaomwamini Yesu Kristo, watashinikizwa kufanya maamuzi ya kukubali au kukataa chapa ya mnyama, iv) Kanisa lazima lijiandae kwa nyakati ngumu zitakazolikabili kwenye dhiki kuu, v) Kanisa litanyakuliwa mwishoni mwa dhiki kuu
UCHAMBUZI WANGU KUHUSU KAMBI ZA UNYAKUO
Kwanza naomba nieleweke kwamba miye sio mshabiki wa kambi za nadharia kwa kufuata mkumbo. Nimefundishwa na kuzoezwa kufanya utafiti binafsi katika maandiko na kupata tafsiri na matumizi sahihi ya maandiko. Sasa inapotokea utafiti wangu ukaangukia kati ya moja wapo ya kambi husika, hiyo haina maana ya kwamba mimi ni mwana-kambi hiyo kwa ushabiki tu.
Kwa mujibu wa kambi za nadhari kuhusu unyakuo, utafiti wangu umejikuta ukiangukia kwenye kambi ya kwanza ambayo ni “Unyakuo kabla ya kipindi cha dhiki kuu” Nimezifuatilia hoja zao na tafsiri ya maandiko nikathibitisha ndivyo yalivyo.
Hata hivyo, ilinichukua muda mrefu kujifunza kwa umakini kuhusu hoja za kambi ya “Unyakuo baada ya dhiki kuu” (Post-tribulation rapture) ili kujua usahihi wa kile wanachoamini, chimbuko la kambi yenyewe na mwelekeo wake kiimani.
Katika utafiti wangu nilikuja kugundua eneo moja kubwa ambalo viongozi wa kambi hii walighafilika na kutoka nje ya tafsiri sahihi na hiyo ikazifanya hoja zao zote nazo kupoteza maana yake halisi.
Eneo hilo kutafsiri ya kwamba, kanisa litakuwepo kwenye dhiki kuu kwa vile limetajwa kwa jina la “wateule” kama tulivyosoma kwenye baadhi ya nukuu za maandiko.
Uchambuzi wangu katika eneo hilo ni kutumia maandiko hayo hayo kuthibitisha kwamba “wateule” wanaotajwa kwenye maandiko husika hayalihusu “kanisa” badala yake yanalihusu “Israeli” kama taifa. Na kama “wateule” ni “Israeli” na sio “kanisa” dhana nzima ya kunyakuliwa baada ya dhiki kuu inapoteza uhalali wake kimaandiko. Hoja zangu za utetezi ni kama ifuatavyo:
1. Mjadala wa mazungumo ulihusu taifa la Israeli
Katika Mathayo 24: Yesu alikuwa anajibu maswali ya wanafunzi wake kwa mtazamo wa Israeli kama taifa na sio kwa mtazamo wa kanisa. Ushahidi ya kwamba aliongea nao kwa mtazamo wa Israeli badala ya kanisa ni maneno yake ya: “ hapo mtakapoliona chukizo la uhabiribu….limesimama katika patakatifu……ndipo walio Uyahudi na wakimbilie milimani…” (MT.24:15-16)
2. Kipaumbele cha huduma ya Yesu kilikuwa ni Israeli
Yesu mwenyewe alikwisha kujitambulisha kwamba ujio wake na huduma yake kipaumbele chake kilikuwa ni kwa taifa la Israeli na sio mataifa: “Akajibu, akasema, sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” (MT.15:24). Na sio kwamba kipaumbele chake ni kwa Israeli kama taifa tu, hata alipowatuma wanafunzi wake ambao wote walikuwa ni wayahudi hakuwapa ruhusa kutembelea watu wa mataifa: “Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” (MT.10:5-6)
3. Katika Ufunuo, Kanisa halitajwi kabisa kwenye kipindi chote cha dhiki kuu
Katika sura tatu za kwanza za kitabu cha ufunuo, Kanisa limetajwa mara kumi na tisa lakini kuanzia Sura za 4-18 ambamo tunasoma taarifa za kina za kipindi cha miaka 7 ya dhiki kuu kanisa halitajwi humo hata mara moja.
Kana kwamba hii haitoshi, kwenye sura ya 3:10 tunakuta Yesu alikwisha kuliahidi kanisa ya kwamba ataliepusha lisiingie kwenye saa ya kujaribiwa kwa ulimwengu: “Kwa kuwa umelishika neno la subira yangu, mimi name nitakulinda, utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote, kuwajaribu wakaao juu ya nchi.”
MWELEKEO WA UNYAKUO KABLA YA DHIKI
Unyakuo wa kanisa kabla ya kipindi cha dhiki kuu ndipo Yesu anapotimiza ahadi ya kuturithisha ufalme wa mbinguni na kuwa pamoja naye mbinguni (Yh.14:1-3) Kunyakuliwa kunajumisha: i) Waliokufa katika Kristo kufufuliwa (1 Thes.4:13-16), ii) Tuliosalia kuvalishwa miili mpya na kunyakuliwa mawinguni (1 Thes.4:17), iii) Kukutana kwenye Kiti cha hukumu cha Kristo kwa ajili ya thawabu mbinguni (2 Kor.5:10), iv) Kushikiri karamu ya arusi ya Mwanakondoo mbinguni (Mt.26:29; Ufu.19:7-9)
Bado mada inaendelea. Najua uchambuzi wangu umetibua sana mitazamo ya kambi ya nadharia za unyakuo. Mimi simo kwenye kambi hata moja ila ninasimamia tafsiri sahihi ya maandiko ambayo yamekuwepo kabla ya kambi za nadharia zilizopo.
Sehemu inayofuata nitaendelea kufafanua ni kwanini “kambi ya unyakuo baada ya dhiki” inasimamia kwamba “wateule” ni “kanisa’’ na sio “Israeli” hata kama maandiko yenyewe wanayosimamia sivyo yasemavyo. Kama umeguswa na mada nisaidie kwa ku-like post hii na kisha uwarushie na marafiki zako. Ubarikiwe sana
Sign up here with your email
1 comments:
Write commentsUNYAKUO KABLA (PRE-TRI)
ReplyHoja za kukataa
1. 2 The 2:7 unajuaje ni kanisa ndo linazuia maana hakuna palipotajwa ni kanisa linazuia
2. Ufunuo 3:10. Unajuaje Hilo kundi la watu wataondolewa kwa unyakuo na sii kwa kupumzishwa labda?? Maana Ufunuo 3, inamakanisa matatu yametajwa hapo na hapo ni kwa mafumbo.
3. Wapi kwenye Agano Jipya kumetaja kutakua na dhiki ya Miaka 7???
4. Je kubadilisha na kufufuliwa kwa wenye haki kuko Mara ngapi?? Jibu ni moja. WATAKAOBAKI kwenye dhiki kuu wakagomea chapa ya Mnyama je watabadilishwa tena baada ya miaka 7 na waliokufa kwa kugoma watafufuliwa tena??? Kwa hiyo kutakua na fufuo 3 pamoja na ile ya mwisho ya wasio haki??? Jibu ni hapana, Imeandikwa kutakua na kubadilishwa Mara moja na ufufuo mmoja wa wenye haki, utakaofata ni baada ya miaka 1000 amabao ni Wa wenye dhambi
Hoja za Post tribulation ni hizi
Ufunuo 20:4-6 inaonyesha Unyakuo utahusisha na waliogoma kupokea chapa ya Mnyama Usoni na mikonoi mwao. Sasa hao wanatoka wapi kama dhiki kuu baada ya unyakuo ndio alama ya mnyama itapigwa???
ConversionConversion EmoticonEmoticon