SEHEMU YA NNE UJUMBE WA KINABII KUHUSU KUNYAKULIWA KWA KANISA UFAFANUZI KUHUSU WATEULE KATIKA MATHAYO 24 NI AKINA NANI..


Bishop Sylvester Gamanywa
Kambi za nadharia kuhusu unyakuo wa kanisa zina malumbano ya karne nyingi kuhusu tafsiri ya msamiati wa neno “wateule” waliotajwa na Yesu Kristo kwenye maandiko ya Injili ya Mathayo 24. Maandiko hayo kama ifuatavyo:
"Na kama siku hizo zisingalifupizwa, asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku hizo." (MT.24:22); "Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule." (MT. 24:24); "Naye atawatuma malaika zake pamoja na sauti kuu ya parapanda, nao watawakusanya wateule wake toka pepo nne, toka mwisho huu wa mbingu mpaka mwisho huu." (MT.24:31; Isa 11:12)
Kwa mujibu wa “kambi ya nadharia ya Kanisa litapitia dhiki kuu” (Post-tribulation rapture) wao wanatafsiri kwamba “wateule” wanaotajwa katika dhiki kuu ni kanisa na sio Israeli. “Kambi ya nadharia ya unyakuo kabla ya kipindi cha dhiki kuu” (Pre-tribulation rapture) wanasema “wateule” wanaotajwa hapa ni “Israeli” na sio “kanisa” kwa kuwa litakuwa limekwisha kunyakuliwa kabla ya dhiki kuanza.
VIGEZO VYANGU VYA UCHAMBUZI
Kama nilivyokwisha kutoa msimamo wangu huko nyuma na hapa narudia tena kuthibitisha ya kwamba, mimi si mshabiki wa kambi za nadharia kwa sababu zote zimeibuka baada ya maandiko yanayobishaniwa yalikwisha kuwepo. Vigezo vya uchambuzi ninavyotumia vinazingatia ukweli wa mambo yafuatayo:
Kwanza, nachunguza ni wakati gani maneno yalioandikwa yalisemwa na ni katika mazingira gani ya wakati huo. Kwa sababu wakati maneno yaliposemwa sio kwamba ndio wakati huo huo yalipoandikwa! Kuna wakati tofauti kati ya "kusemwa maneno" na wakati "maneno hayo yalipoandikwa"!
Pili, nani walengwa wakuu wa maneno yaliyosemwa kwa wakati huo (wayahudi au mataifa?) Hapa pia nazingatia utamaduni wa lugha iliyotumika na jamii ya wakati huo (kiebrania, kiaramu au kiyunani, kilatini nk)
Mantiki ya kuzingatia lugha iliyotumika wakati maneno yaliyosemwa ni kwa sababu lugha iliyotumika kusema maneno husika sio lugha hiyo hiyo ndiyo iliyotumika katika kuyaandika maneno hayo!
Tatu, ni akina nani waliohusika kutafsiri maandiko kutoka lugha asilia iliyotumiwa na waandishi asilia kuja kwenye lugha nyingine! Mfano toka Kiebrania kuja Kilatini au Kiingereza; toka Kiyunani kuja Kiingereza. Pia ni wakati gani kazi ya kutafsiri ilifanyika na kwenye mazingira gani ya kihistoria.
Mwishoni kabisa ndio nakuja kwenye kuzichambua "kambi za shule za nadharia" kuanzia chimbuko la kila nadharia husika kihistoria na kiitikadi. Kwa hiyo utakapoona majibu yangu yakaangukia kwenye msimamo wa mojawapo ya kambi za nadharia nisihukumiwe kwamba miye ni mfuasi wa nadharia hiyo.
Na sasa naanza kutoa uchambuzi wangu kuhusu “wateule” waliotajwa kwenye Injili ya Mathayo 24 ni akina nani? Ni kanisa au Israeli?
WATEULE NI ISRAELI NA SIO KANISA
1. Yesu alitumwa kwanza kwa Israeli kabla ya Kanisa
Mwenye kunishawishi kwa 100% niamini kuwa “wateule” wanaotajwa kwenye MT 24 ni “Israeli’ na sio “kanisa” ni maneno ya Yesu mwenyewe kama alivyojieleza kwenye Injili hiyo hiyo ya Mathayo. Yesu anawataja walengwa wake wakuu wakati wa kipindi chote cha huduma yake akisema: “……Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. “ (MT. 15:24)
Na hata wakati anawatuma wanafunzi wake kwenda kuhubiri kwa mara ya kwanza aliwapa masharti ya kutokwenda kwa mataifa mengine, wala kwa wasamaria: “Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie. Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. (MT.10:5-6)
Kwa mantiki hii, ni dhahiri ya kwamba maneno ya Yesu aliyokuwa kwenye mistari inayotaja “wateule” walengwa wake ni “Israeli” na sio “Kanisa”
2. Dhiki iliyotajwa na Yesu katika Mathayo 24 inahusu Israeli na sio kwa kanisa
Kama nilivyothibitisha hapa juu ya kwamba walengwa wakuu wa Yesu ni “Israeli” na sio “kanisa”; majibu hayo yanaendelea hata kwenye kipengele cha walengwa wa dhiki kuu. Mjadala wenyewe unaanzia kwenye jengo la hekalu. Wanafunzi walipomwonyesha hekalu naye aliwajibu bila kumung’unya maneno akisema:
“ …..Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Basi hapo mtakapoliona chukizo la uharibifu, lile lililonenwa na nabii Danieli, limesimama katika patakatifu (asomaye na afahamu), ndipo walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani;” (MT. 24:2,15-16)
Maneno ya unabii wa Danieli yalitaja moja kwa moja kuwa dhiki italipata taifa la Israeli pamoja na mji wake Yerusalemu (Dan.9:24) Na Yesu mwenyewe anasisitiza kiunabii akisema ikiwafika dhiki “walio katika Uyahudi na wakimbilie milimani.”
Na mahali pengine Yesu anasema kwa kuwahurumia: “Ombeni, ili kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi, wala siku ya sabato.” (MT.24:20)
Kwa kifupi, mazungumuzo kati ya Yesu na wanafunzi wake yenye misamiati ya maneno ya “injili ya Ufalme (24:14), patakatifu (24:15, na sabato (24:20) yote hii inalenga taifa la Israeli na sio kanisa.
Nabii Yeremia yeye alifunuliwa na kuipa jina dhiki kuu hiyo kuwa ni “taabu ya Yakobo”: “Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo. “(YER.30:7)
KANISA HALIKUWEPO WAKATI HUO KWENYE MATHAYO 24
Madai ya kwamba “wateule” waliotajwa katika Mathayo 24 ni “kanisa” na sio “Israeli” ni dhana ya kufikirika bila ushahidi kamili.
Ifahamike ya kwamba, Yesu Kristo alikwisha kusema msamiati kuhusu “kanisa” kwenye Injili hiyo hiyo ya Mathayo. Alipowahoji wanafunzi wake wanamtambua kama nani na Petro akajibu kuwa ni Mwana wa Mungu Aliye Hai ndipo Yesu alitabiri habari za ujio wa kitu alichokiita “kanisa”: “Nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda..” (Mat.16:18).
Muktadha wa msamiati wa lugha kuhusu "kanisa" linalotajwa hapa unalilenga kitu “kitakachokuwepo baadaye” na sio kwamba ni kitu kilichokuwepo kwa wakati huo! Sehemu ya pili ambayo Yesu alitumia msamiati wa neno "kanisa" ni kuhusu mchakato wa kusamehe na kupatana utakaozingatia mara kanisa litakapokuwa limeanza hapo baadaye:
“....na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikilzia kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza ushuru” (Mat.18:17). Maneno haya yoye hayakulenga kuwepo kwa kanisa kwa wakati huo kwa sababu lilikuwa halijakuwepo bado. Yalikuwa ni maelekezo ya Yesu yatakayotumika baadaye.
Kama "wateule" waliotajwa kwenye Mathayo 24 wangelikuwa ni "kanisa" Yesu asingemung'unya maneno angelitaja moja kwa moja kuwa "wateule" hao ni "kanisa"! Lakini kama Yesu hakusema ni "kanisa" maana yake tafsiri ya "wateule" hao sio kanisa.
Kwa mantiki hii maneno mengi yaliyosemwa na Yesu walengwa wake wakuu walikuwa ni kwa Israeli ya Agano la kale na sio Agano Jipya, kwa sababu hata mazingira ya kihistoria ambamo Yesu alikuwa akihudumu yalikuwa ni katika kipindi cha Agano la Kale chini ya torati ya Musa na hekalu ibada za kiyahudi. Agano Jipya limeanza rasmi baada ya kusulubiwa msalabani kufa na kufufuka kwake. Kwa hiyo kabla ya kifo na kufufuka kwa Yesu kanisa halikuwepo.
Sehemu itakayofuata nitajibu kuhusu swali tata la watakatifu katika dhiki kuu ni akina na wanatokana na nini? Ni kanisa ambalo halijanyakuliwa au ni Israeli au ni jamii nyingine? Ikiwa mada hii imekubariki nijulishe kwa ku-like na warushie marafiki zako pia. Ubarikiwe sana
Previous
Next Post »