Bishop Sylvester Gamanywa |
Hii ni
sehemu ya mwisho kuhusu mada hii. Yakiwepo maswali ynayolenga mfululizo
wa mada hii tangu mwanzo ambayo msomaji anaona haijaeleweka nitakuwa
tayari kujibu kwa kifupi kabla ya kufungua mada mpya. Vinginevyo
nimesukumwa kuandika kitabu kinachohusu mada hii na kitakapokamilika
msomaji wa ukurusa huu utakuwa wa kwanza kupata habari zake. Kwa sasa
napenda kufunga mada hii kwa kuelezeka kwa mukhtasari tu kuhusu habari
za DHIKI na mchakato wa mambo yakayojiri siku za mwisho:
TAFSIRI YA DHIKI KINABII
Taabu ya uchungu uliokithiri; mateso makali kupindukia; mazingira
magumu yasiyovumilika. Dhiki ni kipindi ambacho ghadhabu ya Mungu
itamwagwa juu ya ulimwengu uliomkataa Mungu kwa kipindi kirefu tangu
alipomtuma Mwanawe Yesu Kristo kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu.
Walimwengu walichagua uongo badala ya kweli na kuzidi katika uovu sugu
kwa karne nyingi. Mungu alikuwa mvumulivu kwao kwa muda mrefu na sasa
uvumilivu wake utafikia ukomo.
"Kwa kuwa wakati huo kutakuwapo
dhiki kubwa, ambayo haijatokea namna yake tangu mwanzo wa ulimwengu hata
sasa, wala haitakuwapo kamwe. Na kama siku hizo zisingalifupizwa,
asingeokoka mtu ye yote; lakini kwa ajili ya wateule zitafupizwa siku
hizo." (MT. 24:21-22)
"Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari
mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa
taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo
huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana
ameandikwa katika kitabu kile." (DAN.12:1)
KUSUDI LA DHIKI KUU
Kusudi kubwa la kipindi cha dhiki ni kuliandaa taifa l Israeli
kumkubali Masihi ambaye walimkataa wakati alipokuja kwao kwa mara ya
kwanza. Kama ilivyoandikwa ya kwamba: “Alikuja kwa walio wake lakini
hawakumpokea, bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa
Mungu”.(YH.1:11-12) Kwa Israeli kumkataa Masihi, fursa ya neema
ikapelekwa kwa Mataifa mpaka mpaka muda wake utakapokamilika
(Rum.11:25-27)
Kipindi cha dhiki kimetafsiriwa kiunabii kuwa ni
“wakati wa taabu ya Yakobo (Yer.30:7) kwa sababu ni wakati ambapo Mungu
anashughulika na taifa la Israeli. Huu ndio wakati uamsho wa kiroho kwa
wayahudi utasambaa kila kona ya dunia. Wengi watamwamini Yesu na kuanza
kuandaa kizazi kipya cha Israeli watakaoingia kwenye utawala wa milenia.
Mungu atatimiza unabii wa juma moja ili kutimiza kusudi lake kuhusiana
na Israeli (Dan.9:24)
Ni wakati wa dhiki hata mataifa wasio
wayahudi nao watamwamini Yesu kupitia Injili ya Ufalme itakayohubiriwa
na wale wayahudi 144,000. Hawa mataifa watakaookolewa wakati wa dhiki
kuu na ambao hawatakufa kwenye dhiki ndio watakajumuika kama kondoo
kwenye hukumu ya Kristo kama ilivyotabiriwa kwenye Mathayo 24.
Kusudi la pili la dhiki ni Mungu kumwaga ghadhabu yake juu ya walimwengu
ambao waliikataa Injili wakati wa kipindi cha kanisa la Kristo kabla ya
dhiki kuanza. Wengi wakati huu watakuwa wamejisajili chini ya utawala
wa Mpingakristo na kushikiri maovu yaliyokithiri na ghadabu ya Mungu
atashuka kwa ajili yao ili kupatiliza maasi yatakayokuwa yakiendelea
kila mahali duniani kwa wakato huo. (2 Thes.2:11-12) Kusudi la tatu la
dhiki ni kufanya hukumu dhidi ya kanisa lililokengeuka ambalo litakuwa
likiongozwa na Nabii wa uongo (Ufu.17:6) Ufu.17:15-18
MCHAKATO WA MAMBO KATIKA DHIKI
Baada ya kunyakuliwa kwa Kanisa, na utendaji wa Roho Mtakatifu kutoweka
juu ya uso wa dunia hii, ndipo ukengefu wa kiimani na mmomonyoko wa
maadili utakithiri kupindukia. Kiwango cha uasi dhidi ya mamlaka
zilizoko kitapanda na kupoteza amani ya kijamii na uhuru wa kuabudu
Mungu wa kweli utatoweka katika jamii. Uvunjwa wa amri za Mungu katika
Biblia utakuwa ndio mtindo wa maisha ya kila siku katika jamii. Wakati
huo hakuna tena Injili ya wokovu kwa kuwa aliyekuwa mtetezi wake hayupo
tena duniani. (Hivi sasa yuko azuiaye)
Kutokana na mkenguko
mkubwa wa kiimani na kimaadili katika dunia nzima, Shetani atatumia
fursa hiyo kumtambulisha wakala wake ambaye ni Mpingakristo ambaye
atajitokeza kuwa ni mpatanisha na mtatuzi wa matatizo ya kisiasa,
kiuchumi na kidini ambayo yatakuwa yanasumbua dunia nzima. Huyu Mpinga
Kristo atavuviwa na shetani katika kufanya hata miujiza ya uongo ili
kuwadanganya walimwengu ambao waliikataa Injili ya kweli wakati kanisa
la kweli la Kristo lilipokuwa bado liko duniani. (2 Thes.2:9-10)
Mojawapo ya miujiza mikubwa atakayofanya huyu Mpingakristo ni
kufanikisha zoezi la kusaini mkataba wa Amani kuhusu mgogoro sugu wa
Mashariki ya Kati, kati ya Israeli na Waarabu. (Dan.9:27) Mojawapo ya
ushawishi wake kwa Israeli ni kukamilisha hitaji la ujenzi wa Hekalu la
kiyahudi na wayahudi wataanza kutoa dhabihu za wanyama kama zamani. Na
pia atafanikisha zoezi la kuundwa kwa serikali moja ya ulimwengu mzima
ambapo mamlaka za mataifa binafsi yatajumuishwa pamoja chini ya utawala
wa mfumo wa serikali moja ya dunia.
Wakati huo atatokea mtu
mwingine mwenye ushawishi mkubwa katika mambo ya uchumi na dini
(Ufu.13:11-17) Kazi ya mnyama huyu kwa jina maarufu la Nabii ya uongo
atakuwa mpiga debe wa Mpingani Kristo katika kuhamasisha ulimwengu
kumwabudu Mpingakristo sawa na Mungu. Atafanya ushawishi mkubwa kwa njia
ya kuweka mfumo mmoja wa uchumi ambapo kila raia duniani atawajibika
kujisajili kwenye mfumo huo ilia pate kufanikisha mambo yake ya
kiuchumi.
AWAMU YA PILI YA DHIKI
Baada ya kipindi cha
miaka mitatu na nusu ndipo awamu ya pili ya dhiki itaanza kwa
Mpingakristo kuvunja mkataba wa amani aliofanya Israeli na waarabu.
Mkataba huo utavunjwa kwa Mpingakristo kuingia kwenye hekalu na
kujitangaza kuwa yeye ndiye Mungu na wayahudi wamwabudu yeye. Hilii
ndilo linaitwa “chukizo la uharibifu” (Dan.9:27; 2 Thes.2:3-10)
Hii awamu ya pili ya dhiki ndiyo inaitwa DHIKI KUU, (Ufu.7:14) na ndiyo
inaitwa “wakati wa taabu ya Yakobo (Yer.30:7) Kilele cha dhiki kuu
kitafikiwa pale ambapo Mpingakristo ataongoza vita ya kuiangamiza
Israeli kuanzia Yerusalemu maarufu kwa jina la VITA YA ARIMAGEDONI.
Kabla ya kutimiza mkakati huo ndipo Yesu Kristo mwenyewe ataamua kurudi
mara ya pili duniani na majeshi yake ya Mbinguni na kuja kumwangamiza
Mpingakristo na majeshi yake na kuwatupa kwenye ziwa la moto
(Ufu.19:11-21)
Kazi ya Yesu pia itakuwa ni kumkamata Shetani
mwenyewe na kumfunga kwenye shimo la giza kwa kipindi cha miaka 1000
(Ufu.20:1-6); na kisha Yesu kuweka utawala wa milenia, na makao makuu
yakiwa jijini Yerusalemu.
Nachukua fursa hii kuwashukuru wote
mliofuatilia mada hii na kujibu kwa njia mbali mbali. Natarajia kwamba
tutaendelea kuelimishana kwenye mada mpya zinazokuja mbeleni. Mbarikiwe
sana.
Sign up here with your email
ConversionConversion EmoticonEmoticon